Dar es Salaam. Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mohamed Mpinga amesema kikosi hicho kipo kwenye mkakati maalumu wa kuondokana na kero ya malori yanayoegeshwa ovyo katika maeneo ya hifadhi ya barabara jijini Dar es Salaam.
Kamanda Mpinga alisema kwa kuanzia askari wa kikosi hicho wamefanikiwa kuondokana na adha ya malori yaliyokuwa yakiegeshwa ovyo katika eneo la reli Ami.
“Tumefanikiwa kukabiliana na changamoto hiyo katika eneo sugu la reli Ami na tumepiga marufuku malori kuegeshwa kwenye hifadhi ya barabara”alisema
Kamanda Mpinga alisema ameagiza wakuu wa usalama barabarani wa maeneo mengine kuchukua hatua za haraka dhidi ya madereva wa malori yanayoegeshwa ovyo ikiwa ni pamoja na kubandua namba za usajili.
“Wakati mwingine madereva wanaegesha magari yao na kujificha sasa nimeagiza yang’olewe namba za usajili hapo nina uhakika dereva mwenyewe atajileta kituoni”alisema Kamanda Mpinga
Kwa muda mrefu tatizo la malori limekuwa likipigiwa kelele na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kutokana na magari hayo kuegeshwa ovyo, hali inayosababisha ajali za mara kwa mara pamoja na usumbufu mkubwa wa foleni katika maeneo mbalimbali na hasa katika barabara za Mandela na Morogoro.
Aidha Kamanda Mpinga ameendelea kuhimiza matumizi bora ya barabara kwa madereva wa vyombo vya usafiri kwa kuzingatia sheria za barabarani ili kuepukana na ajali.
No comments:
Post a Comment