SAFU yetu ya Mwanasiasa wa Wiki leo imebahatika kufanya mahojiano na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa upande wa Zanzibar, Saidi Issa Mohamed, muda mfupi kabla hajapanda ndege kwenda nje ya nchi kwa shughuli za chama.

Miongoni mwa mambo anayoelezea Mohamed ni pamoja na namna walivyompata mgombea wa nafasi ya urais mwaka 2010 na suala zima la udini, ukanda na ukabila unaodaiwa kuwamo ndani ya chama chake.

Swali:
Unazungumziaje suala la chama chenu kudaiwa kuwa na udini, ukabila na ukanda? Dini yenyewe inayozugumzwa ikiwa ni Ukristo wa madhehebu ya Katoliki na inasemekana mmewekwa pale kwa ajili ya kuficha madai hayo?

Mohamed: Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukuongoza kuniuliza hayo, hapo kuna maswali matatu, nitakujibu kila swali kwa nafasi yake, nikianza na suala zima la udini.

Kama watu wanafuatilia historia ya kuanzishwa kwa vyama vingi na wakaamua kukataa propaganda zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali nzima basi watabaini kuwa hakuna kitu kama hicho kwa Tanzania, ila waliofilisika kisera wanataka kutumia turufu hiyo ya udini kama nafasi ya kuonewa huruma katika jamii.

Nasema hivyo kwa sababu mtiririko mzima wa uongozi ndani ya CHADEMA, kuanzia kuasisiwa kwake haukuwa wa kuangalia dini bali uwezo wa mtu, na katika hili linadhihirishwa na namna uongozi ulivyokuwa tangu mwanzo hadi sasa, mwenyekiti wa kwanza wa CHADEMA alikuwa mzee Edwin Mtei.

Huyu ni Mkristo na katibu mkuu alikuwa mzee Ally Nyanga Makani ‘Bob Makani’, huyu ni Mwislamu, naibu wake kwa Bara alikuwa mzee Saidi Arfi, naye huyu ni Mwislamu na kwa viongozi waliotoka Zanzibar wote walikuwa Waislamu.

Awamu ya pili, mwenyekiti alikuwa Bob Makani, makamu Dk. Willbrod Slaa na katibu mkuu alikuwa Amani Walid Kabourou.

Awamu ya tatu, mwenyekiti wetu alikuwa Freeman Mbowe, makamu Kabourou, katibu mkuu, Dk. Slaa, katika nafasi ya makamu mwenyekiti hapa alikuwa Shaibu Akwilombe na baadae akawa Chacha Wangwe (marehemu).

Awamu hii tunayokwenda nayo sasa, Mbowe ameendelea kuwa Mwenyekiti, Makamu wake Bara ni Said Arfi, Zanzibar ni mimi, Katibu Mkuu ni Dk. Slaa, Naibu wake Bara ni Zitto Kabwe na Zanzibar ni Hamad Yusuph, hapa utaniambia Ukristo na huo Ukatoliki uko wapi?

Pia ukiangalia namna viongozi walivyo kuanzia mwanzo, hakuna safu nzima ya viongozi wakuu waliotoka kanda moja au kabila moja.

Kama kungekuwa na udini katika CHADEMA huo unaosemwa, basi Waislamu wasingepita na kuwa katika nafasi walizonazo leo, kwa kuwa nafasi zote za juu ni za kupigiwa kura.

Swali: Sasa unafikiri kwanini mambo hayo yanazungumzwa kuhusu ninyi na si vyama vingine?

Mohamed:
Sasa hivi CHADEMA tupo katika mioyo ya watu na hili ni tishio kwa chama tawala, kama utakumbuka wakati ule CUF ilipokuwa juu waliambiwa ni chama cha kigaidi, cha Waislamu na mwisho kikaitwa cha Wapemba, nao walikubaliana na propaganda hizo pasipo kujua kuwa zinawamaliza, unaona leo wameshuka wale waliowazushia hawaoni tishio la CUF tena, sasa wameivamia CHADEMA.

Hii ni baada ya kutangazwa Kwa Dk. Slaa kuwa mgombea wetu mwaka 2010, lengo lilikuwa kuwagawa wananchi na kisha wawatawale, serikali inafanya hivi makusudi kwa kutumia idara zake za usalama ambao hawataki kutambua kuwa wapo kwa ajili ya masilahi ya taifa na si chama cha siasa.

Watanzania wanapaswa wajiulize kama CHADEMA kinasemwa ni cha Wakristo, CUF ya Waislamu na CCM itakuwa ya dini gani? Au hao wenye dini hizo zinazotajwa kuwa ni za CUF na CHADEMA wanajipendekeza ndani ya CCM?

Swali:
Umehusisha idara za usalama kushiriki katika propaganda hizi na wao wanashiriki vipi? Wakati taarifa za chama hicho kuwa cha kidini zilikuwa zinatolewa katika nyumba za ibada?

Mohamed:
Fahamu kuwa idara ya usalama ina watu wengi katika maeneo tofauti ya kijamii, hili la kusemwa kanisani au msikitini lisikupe taabu, kwani hata huko wana watu wao na ndio wanaokuwa wa kwanza kupokea tamko la uchonganishi kutoka katika dini nyingine na kulifikisha kwa waumini wao, katika mtazamo wa kawaida unaweza ukasema ni Wakristo au Waislamu ndio wamesema kumbe hilo limefanywa na watu waliokaa meza moja na kutengeneza ajenda ya kuwagawa Watanzania.

Sitaki kuwa mtabiri juu ya hili la kuwagawa watu kiimani kwa ajili ya kutaka kuungwa mkono katika uchaguzi, ni wazi sasa hata waliolianzisha limewashinda, imekuwa ni silaha ambayo mtaalamu wake ameshakufa na waliobaki hawana ujuzi wa kulifanya lisilete madhara. Ninamuomba Mwenyezi Mungu Watanzania wasifikie katika hali ya kushikana mashati kwa ajili ya imani zao.

Swali: Kwanini unakataa kuwapo kwa suala la udini, ukanda na ukabila ndani ya CHADEMA wakati wapinzani wenu wanalihusisha hilo na namna mlivyowapata wabunge wa viti maalumu? Kwani idadi kubwa inaonekana kutoka Kanda ya Kaskazini, hili huoni kama linadhihirisha suala zima la ukanda na ukabila?

Mohamed:
Binafsi kabla ya kuja CHADEMA nilikuwa mwanachama wa CUF, ninajua namna viti maalumu vinavyopatikana na huu utaratibu uliotumiwa na chama changu baada ya kuharibika uchaguzi mkuu wa baraza la wanawake ninasema ni mzuri na hauna tatizo lolote.

Swali: Mzuri vipi? Unaweza kunifafanulia huo uzuri unaousema na kuondoa shaka iliyojengeka kuwa nafasi zilikuwa za kupeana?

Mohamed: Tuliweka vigezo zaidi ya sita ambavyo havikuangalia imani ya mtu wala ni wapi mtu anatoka na kila kigezo kilikuwa na alama zake, hivyo waliofanikiwa kuwazidi wenzao kwa hivyo vigezo ndio walikuwa katika nafasi nzuri ya kuingia katika viti maalumu; navyo ni elimu, uzoefu wa aina yoyote katika kuitumikia jamii, mchango wa mhusika katika chama hapa ni wa hali na mali, na muda aliojiunga. Hivi ni kwa uchache, lakini nikuhakikishie hata wale waliokuwa ni makada wasaidizi waliweza kuongeza alama zao kwa uzoefu huo na wengine leo ni wabunge kupitia vigezo hivyo.

Swali: Tayari Tanzania imeshafanya uchaguzi mkuu wa wabunge na rais katika vipindi vinne, ambapo vyama vya upinzani vilishiriki na ninyi ndani ya CHADEMA mmeshiriki katika awamu zote hizo na kusimamisha wagombea wa urais mara mbili, je, mwanzoni hakukuwa na watu wa kuweza kugombea nafasi hizo?

Mohamed: Mwaka 1995 tulimuunga mkono mgombea wa urais kutoka chama kimoja kilichokuwa na nguvu wakati huo, mwaka 2000 ilikuwa tusimamishe mgombea wa nafasi ya urais na alikuwa ni mwanamke, cha kutusikitisha dakika za mwisho tuliyemtegemea akaamua kuachana na nia hiyo, mwaka 2005 mtakumbuka kulikuwa na mvutano mkubwa wa kuwania nafasi ndani ya CCM, nasi tulimuandaa Profesa Mwesiga Baregu, lakini mpaka dakika za mwisho sekretarieti ikawa haina taarifa zake na hata alipopatikana hakuwa tayari kugombea vile vile, tukaamua kumweka Mbowe, hakutaka, ila tulimlazimisha kwa ajili ya kukiweka chama mioyoni mwa watu, naye alikubali na akaachana na nia ya kugombea ubunge kule Hai.

Swali: Niambie namna mlivyompata Dk. Willibrod Slaa kuwa mgombea wenu na kuna madai kuwa aliwapa sharti la kumlipa mshahara anaoupata katika ubunge endapo angekosa nafasi ya urais mwaka 2010?

Mohamed:
Kwanza nikurejeshe kidogo katika harakati za kumpata mgombea wa chama chetu mwaka 2010, kwa asilimia kubwa tulijua Samuel Sitta angesimama kwa ajili ya CHADEMA na mawasiliano hayo tulikuwa nayo hadi muda unakaribia wa kupeleka majina ya wagombea, lakini Sitta akatugeuka dakika za mwisho. Hii inaonesha namna ndani ya CHADEMA tusivyokuwa na tamaa ya kugombea urais bali tunataka ufanisi.

Baada ya Sitta kutugeuka tukasema tunao watu wetu, tena ni wazuri na wanaaminiwa na wananchi, vijana na wasomi mbalimbali wakaingia mikoani kufanya utafiti ni nani anaweza kusimama kwa ajili ya CHADEMA, jibu likaja kuwa ni Dk. Slaa.

Ugumu ukawa namna ya kumshawishi aachane na ubunge, kwa kuwa alikuwa amekwisha kuchukua hadi fomu kugombea ubunge katika Jimbo la Karatu. Tulijadiliana wenyewe kwanza kabla ya kumwambia kuwa kamati kuu itamteua, na Mwenyekiti Mbowe alifanya hili kuwa siri kubwa kwa Dk. Slaa na hapo ndipo tulipomshitukiza.

Baada ya kumshitukiza Dk. Slaa kama unavyomjua, kwanza alishangaa na hakuwa na jibu la kusema. Lakini nikuambie, hapa kulitokea mtafaruku. Mjumbe wa kamati kuu, huyu bwana anaitwa, Maasey, anatoka Karatu, alisimama kwa ghadhabu na kuuliza, kwanini katika hili hatujawashirikisha watu wa jimbo lake. Kwa kweli ulikuwa mtafaruku, hadi akasema kama tumeamua kumfanya Dk. Slaa kuwa mgombea urais wa CHADEMA, wao Karatu wanahamia CCM.

Hii yote ni kwa mapenzi na uwajibikaji wa Dk. Slaa, ndiyo maana kila mmoja akataka kuwa karibu yake. Kiutendaji wao Karatu waliona wanampoteza mchapakazi katika jimbo lao, lakini tuliwafahamisha kuwa kwa masilahi ya nchi na chama ni vema wakubaliane na uamuzi wa kamati kuu.

Suala likaja, je, kama atashindwa tutamuwajibikia vipi? Napo tukakaa chini na kufanya tathmini kuwa huyu kwa Karatu anapita kwa asilimia 100 na kama ikitokea akashindwa katika nafasi ya urais, basi tumlipe mshahara wa ubunge. Haya ni makubaliano ya wote, si kwamba Dk. Slaa alilazimisha.

Baada ya kujadiliana hili kwa pamoja ikatulazimu kuunda timu ya kwenda Karatu kuwaelezea umuhimu wa wao kumwachia Dk. Slaa kuwa kinara wa kuivusha CHADEMA katika hatua iliyokuwapo, nao wakatuelewa na wakatuahidi jimbo hawatalirudisha kwa CCM, kweli walitimiza ahadi yao, watu wale ni waaminifu katika ahadi zao.

Majibu kwa wanaodai Dr. Slaa alilazimisha mshahara mkubwa CHADEMA