Pages

Sunday 28 July 2013

Halmashauri Morogoro yaburuzwa kortini


HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imeingia matatani ikidaiwa fidia ya shilingi mil. 60 na Kampuni ya Mkomilo Trade Centre Ltd iliyoingia mkataba wa kukusanya ushuru kwenye soko la Mawenzi mjini hapa baada ya kuusitisha kinyemela.
Fidia hiyo iliyoilazimu kampuni hiyo kwenda mahakamani chini ya Kampuni ya uwakili ya Emanuel M. Augustino ya jijini Dar es Salaam inatokana na kuahirisha mara kadhaa huku kampuni hiyo ikiendelea kupata hasara kubwa kila mwezi kutokana na gharama ilizoingia kununua vifaa na inazoingia ikiwamo kuendelea kuwalipa wafanyakazi walioajiriwa kwa kazi hiyo.
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Moris Makoi, alisema hasara hiyo ni pamoja na dhamana ya zaidi ya shilingi 800,000, faida ambayo kampuni ingepata kwa kipindi hicho, gharama za uendeshaji ofisi na vifaa, malipo kwa watumishi na gharama za kuendeshea kesi.
“Si nia yetu kudhalilishana lakini imefikia hapa kutokana na ukweli kuwa mimi naendelea kuumia huku sijui hatima yangu, fikiria ingawa tayari nimeshinda tenda napokea barua kila kukicha ya kusitisha kazi, nikifika ofisini majibu ni mepesi, ‘ngoja tunashugulikia au utaanza mwezi ujao au subiri’”, alisema Makoi.
Baadhi ya barua za manispaa hiyo zilizosainiwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Jolvis Simbeye, kusitisha kwa muda mkataba huo ni yenye kumbukumbu namba LGA/079/2012-2013/NS/06/02 na barua ya Februari 28, kumbukumbu namba C20/MMC-1/Vol.VII/63 ya Mei 31, kumbukumbu namba T.10/MMC-10/78 na ya Juni 13, yenye kumbukumbu namba T10/MMC-10/81.
Barua hizo ambazo hazima maelezo yanayoonyesha mzabuni atakavyofidiwa ghama anayoipata zimeeleza dhamira ya kusitishwa kwa mkataba huo kuwa ni kutokana na vurugu za wafanyabiashara wanaopinga ushuru huo wakidai hauwanufaishi huku wakiituhumu manispaa kufuja fedha za soko hilo kutokana na mapato yanayotajwa kukusanywa sokoni hapo kuonekana kidogo.
Mkurugenzi wa halmashuri hiyo, Jolvis Simbeye, pamoja na kukiri kuingia mkataba wa kisheria na kampuni hiyo, alisema manispaa ilifanya hivyo kuepusha vurugu inayoweza kutokea ofisini sokoni hapo pindi mzabuni huyo akitekeleza majukumu yake.
“Labda nieleze kuwa tumekuwa tukimwandikia barua hizo kutokana na hali mbaya iliyopo katika soko lile, sisi wenyewe tunapoteza mapato sasa hivi maana hakuna tunachokusanya pale, lakini tumesha mweleza kupitia vikao vyetu na tumekubaliana kuwa aanze kazi tarehe 1/8/2013 na Jumatatu tutampa barua aanze,” alisema Simbeye.
Kuhusu uvumi kuwa tayari kazi hiyo wamepewa umoja wa wafanyabiashara sokoni hapo kukusanya ushuru huo, Simbeye alikanusha akidai si jambo rahisi kufanya hivyo kwa sababu mbalimbali ikiwamo mchakato wa mtu kupata tenda ni lazima iwe kampuni iliyosajiliwa na lazima waonyeshe uzoefu wa kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment