Pages

Monday 29 July 2013

MBEYA:BABA JELA MIAKA 30 KWA KUZAA NA MTOTO WAKE MWENYEWE

MAHAKAMA ya Mkoa wa Mbeya imemhukumu kifungo cha Miaka 30 jela Mkazi wa Isanga Jijini Mbeya, Hamad Yusufu, kwa kosa la Kuzini na Binti yake na Kuzaa naye mtoto mmoja wa Kike.

Baba huyo anadaiwa kuanza kuzini na binti yake mwaka 2008 akiwa na umri wa miaka 11 akimtisha kwa kutumia panga na kumpa ujauzito miaka mitano baadaye na kusababisha akatishe masomo ya elimu ya msingi.


Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Gilbert Ndeuruo, amesema Mahakama imezingatia zaidi ushahidi uliotolewa na mtoto wa mshitakiwa huyo, Hadija Yusufu, anayedaiwa kuzini na kuzaa naye mtoto mmoja, Eva Yusufu, aliyethibitisha bila shaka kuwa baba yake alimlazimisha kuzini naye akimtishia kwa panga kwa zaidi ya miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2012, alipopata ujauzito.

Pia Hakimu Ndeuruo, amesema mahakama hiyo imeridhika bila shaka kuwa mshtakiwa Hamad amefanya kosa hilo baada ya vipimo vya vinasaba yaani DNA vilivyowasilishwa Mahakamani hapo na Afisa kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Hadija Said Mwema, kuonesha kuwa mshtakiwa huyo amefanana na mtoto Eva aliyezaliwa na binti yake Hadija, kwa asilimia 99.9.

Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka, ulioongozwa na Mwendesha Mashtaka Lugano Mwakilasa, mshitakiwa huyo ameanza kuzini na binti yake mwaka 2008 akiwa darasa la Tano baada ya kuachana na mkewe, Regina Simon, aliyefunga naye ndoa mwaka 1997 mkoani Mbeya.

Hata hivyo, mshitakiwa huyo ameonesha nia ya kukata rufaa kupinda adhabu hiyo licha ya kushindwa kuitumia fursa ya kuomba punguzo la adhabu aliyopewa na Hakimu Ndeuruo, akidai anaiachia mahakama ifanye itakavyo kwa madai hakufanya kosa hilo bali kesi hiyo imetokana na chuki alizonazo mke wake, Regina Simon, baada ya kuachana.

Nje ya Mahakama, baadhi ya wananchi wametoa maoni yao kuhusu adhabu hiyo.

Hukumu hiyo ni ya pili kutolewa na Mahakamani hapo katika kipindi cha Julai mwaka huu kuhusu makosa ya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya watoto wa kike, ambapo hukumu ya kwanza imetolewa na Hakimu Ndeuruo Julai Mbili mwaka dhidi ya Mchungaji wa Kanisa la Evangelical Assemblies of Gog, EAGT, mkoani Mbeya, Daniel Mwasumbi, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka na kumpa ujauzito mara mbili mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Itende mjini hapa, Neema Benson.

No comments:

Post a Comment