Pages

Tuesday, 23 July 2013

CHADEMA YAWANG'ANG'ANIA MADIWANI WALIOTIMULIWA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimefungua kesi ya madai, yenye gharama zaidi ya Sh. milioni 35.1 dhidi ya waliokuwa madiwani wake watano, waliofukuzwa jimbo la Arusha Mjini.

Madiwani hao ni Charles Mpanda (Kaloleni), John Bayo (Elerai), Estomih Mallah, (Kimandolu), Rehema Mohamedi (Viti Maalumu) na Reuben Ngowi (Themi).

Chadema wamefungua madai yao kupitia wakili wao, Method Kimomogolo na yanatarajiwa kutajwa kesho mbele ya msajili wa wilaya, Mahakama Kuu kanda ya Arusha, Wilbad Mashauri.

Kesi hiyo inatokana na hatua ya madiwani hao, kushindwa kuhudhuria kwenye kesi yao, walilofungua mahakama kuu kanda ya Arusha, mbele ya Jaji Kakusolo Sambo, wakiiomba ifanyie mapitio uamuzi wa kulipagharama za kesi, uliotolewa na aliyekuwa hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Arusha, Charles Magesa.

Hata hivyo, Jaji Sambo aliamua kesi hiyo kwa kufuta shauri hilo Aprili 02, mwaka huu, baada ya madiwani hao kutoonekana mahakamani hapo, bila taarifa mara mbili mfululizo na aliwataka kulipa gharama za usumbufu.

Novemba 22, 2012 Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha iliwaamuru madiwani hao waliotimuliwa Chadema kulipa zaidi ya Sh. milioni 15 na kila mmoja alitakiwa kulipa Sh. milioni 3.1 ndani ya miezi miwili, kama gharama za kesi waliyokuwa wamefungua, kupinga kufukuzwa uanachama, vinginevyo watapelekwa magereza.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Charles Magesa alitoa hukumu hiyo baada ya Chadema kushinda kesi hiyo na kuwaamuru kulipa Sh. milioni 15 ndani ya miezi miwili, wakishindwa watapelekwa gerezani.

Hata hivyo tayari wadaiwa hao walishalipa deni hilo, isipokuwa John Bayo, ambaye anadaiwa Sh. 507,000 na Mpanda anayedaiwa Sh. milioni 1.5 na tayari mahakama hiyo, ilishatoa hati ya kukamatwa kwao toka Februari 19, 2013.

Katika shauri hilo, Wakili Kimomogolo alisema kuwa, wateja wake (
CHADEMA) walishawasilisha mahakamani hapo fedha kwa ajili ya kuwahudumia waliokuwa madiwani wakiwa gerezani.

Madiwani hao walitimuliwa
CHADEMA baada ya kuingia muafaka wa kiti cha umeya wa Jiji la Arusha, bila kupata baraka za chama.

CHANZO: NIPASHE
 
Mbunge G. lema,Arusha mjini

No comments:

Post a Comment