TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, inaweza kufananishwa na sikio la kufa ambalo kamwe huwa halisikii dawa, licha ya juhudi kubwa za kusaka tiba.
Ndivyo ilivyo kwa timu hiyo ambayo baada ya Juni 8 kupoteza nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, jana imeshindwa tena kupata tiketi ya fainali za Afrika kwa nyota wa Ligi za Ndani-CHAN.
Kipigo cha siku hiyo cha mabao 4-2 kutoka kwa Ivory Coast kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kikafuta hesabu za Brazil, hivyo turufu pekee ilikuwa ni fainali za CHAN nchini Afrika Kusini, pia za mwakani.
Katika mechi ya jana iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Mandela, mjini Namboole, nje kidogo ya Kampala, Stars wakiwa nyuma kwa bao 1-0 walilofungwa Julai 13, jijini Dar es Salaam, walifungwa tena 3-1.
Kwa idadi ya mabao 4-1, si tu imeitupa Stars nje ya vita hiyo ya kwenda Brazil na kuipa Uganda tiketi ya Afrika Kusini, pia imetoa jawabu kwamba kazi kubwa inahitajika ili kuwa na timu bora.
Stars iliyocheza fainali za kwanza nchini Ivory Coast mwaka 2009 chini ya Mbrazil Marcio Maximo, ilimaliza kipindi cha kwanza kwa sare ya bao 1-1.
Wenyeji walianza kufunga bao dakika ya saba katika mechi iliyochezeshwa na Kanoso Abdoul Ohabee kutoka Madagascar, likifungwa na Frank Kalanda, akimalizia mpira uliopigwa ndani ya eneo la hatari la Stars.
Bao hilo liliwafanya Stars watulie zaidi na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 18, mfungaji akiwa Amri Kiemba kutokana na pasi nzuri ya Mrisho Ngasa kwenye kona ya eneo la mita 18.
Dakika ya 32 nusura Stars ipate bao, lakini mkwaju maridadi wa Ngasa ambao tayari ulikuwa umempira kipa Hamza Muwonge, uligonga mwamba kabla ya kuokolewa na mabeki.
Bao la pili la wenyeji katika mechi hiyo lilifungwa dakika ya 48 na Brian Majwega, kabla ya Kalanda kuongeza la tatu dakika ya 63, kutokana na makosa ya Salum Abubakar kupokwa mpira akiwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa pasi kwa mwenzake.
Kocha Kim Poulsen alifanya mabadiliko dakika ya 43, akimwingiza Simon Msuva badala ya Frank Domayo aliyeumia na dakika ya 78 akawaingiza kwa mpigo Haruna Chanongo na Vincent Barnabas na kuwatoa David Luhende na John Bocco.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadili matokeo ya mchezo ambapo hadi mwisho wenyeji Uganda waliibuka na ushindi wa mabao 3-1, hivyo kujitwalia tiketi ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1.
Kikosi cha Stars kilipangwa hivi: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende/Vincent Barnabas, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Frank Domayo/Simon Msuva, Salum Abubakar, John Bocco/Haruni Chanongo, Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itarejea nyumbani leo saa 4 usiku kwa ndege ya Precision Air.
No comments:
Post a Comment