WANAJESHI saba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa wakati wakilinda amani Darfur nchini Sudan, walipigana kwa saa mbili wakati wakijitetea kabla ya kufikwa na mauti.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati akitoa salamu za rambirambi, wakati wa kuaga askari hao waliouawa Julai 13.
Katika shughuli hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), Rais Jakaya Kikwete aliongoza waombolezaji kuaga mashujaa hao ambapo pia Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal na mawaziri mbalimbali walihudhuria.
“Kikundi hicho (askari wa JWTZ) kilikuwa kikitokea eneo la Abeche, kwenda Nation na kilipofika umbali wa kilometa 25, doria hiyo ilipunguza mwendo kutokana na utelezi wa matope yaliyosababishwa na mvua.
“Ghafla kikundi hicho kilishambuliwa na watu ambao hawakufahamika, wakitumia silaha nzito za kivita,” alisema Jenerali Mwamunyange.
Alisema ulikuwa ni mtego wa mashambulizi na kwa mujibu wa taratibu za operesheni hizo, doria hiyo haikuwa na silaha nzito, lakini ililazimika kujibu mapigano hayo hadi kikundi kingine cha askari wa JWTZ, kilipoitwa kuongeza nguvu kunasua wenzao katika mtego huo.
Jenerali Mwamunyange alisema wakati kikundi hicho kikinasuliwa, askari hao walipoteza maisha kwa ujasiri mkubwa na wengine 14 kujeruhiwa.
Alisema Tanzania imefikwa na msiba huo wa mashujaa, ikiwa imeshiriki kulinda amani Sudan tangu mwaka 2007, ambapo askari wake wamekuwa wakitekeleza majukumu yake kwa weledi wa hali ya juu, kwa kushirikiana na vikundi vingine na wenyeji katika maeneo ya operesheni.
Majina yao Awali Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alitaja majina ya mashujaa hao na mahali wanapokwenda kuzikwa, kuwa ni pamoja na Sajini Shaibu Othman (Zanzibar) na Koplo Osward Chaulo (Kilolo, Iringa). Wengine ni Koplo Mohammed Ally (Zanzibar), Koplo Mohammed Chukulizo (Kigoma), Praiveti Rodney Ndunguru (Songea), Praiveti Fortunatus Msofe (Tanga) na Praiveti Peter Werema (Tarime, Mara).
Rais Kikwete alisema mauaji ya wanajeshi hao, yalimshitua, kumhuzunisha na kumkasirisha na kujikuta akijihoji kwa nini watu wa Sudan waue Watanzania.
Alisema Watanzania hao walikwenda kuwasaidia kupata amani, utulivu, kunusuru maisha yao na kuwaondolea mazingira ya wasiwasi ili wafanye shughuli zao kwa tija.
Alisema tangu kuanza kwa shughuli za ulinzi wa amani Darfur, walinzi wa amani 41 kutoka mataifa mbalimbali wameuawa, na 55 kujeruhiwa na hakusita kuamini kuwa waliofanya tukio hilo ni wasiotaka amani Darfur.
“Idadi hii ni kubwa, inahitaji kutafakari vizuri na kutazama upya mfumo wa kiwango cha kujilinda kwa wanajeshi… lazima uwezo huo uongezwe ili kupunguza vifo zaidi,” alisema Rais Kikwete.
Aliahidi kufikisha maombi hayo kwa Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN), ili walitazame vizuri. Mchango wa Tanzania Rais Kikwete alisema Tanzania tangu Uhuru imekuwa ikijitolea kusaidia wanyonge dhidi ubaguzi, uonevu na wengine ambao njia za diplomasia zimekuwa zikitumika.
Aidha, alisema wakati wote walipoombwa, walijua uwezekano wa askari wao kujeruhiwa au kupoteza maisha, ni mambo yaliyofikiriwa kuwa yanaweza kutokea kwani walikwenda kwenye maeneo ya hatari, yenye mapigano.
Alisema kutokea hayo si ajabu, lakini hadhari kubwa ilichukuliwa kwa kupewa mafunzo, zana za kujihami, kujilinda na kutekeleza majukumu.
Rais Kikwete alisema baada ya mauaji hayo ya Darfur alizungumza na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon ambaye alielezea masikitiko yake na kutoa pole nyingi, na kueleza kwamba alizungumza na Rais wa Sudan, Omar Al-Bashir, ili achukue hatua ya kusaka na kuwaadabisha wahalifu hao.
“Nami pia nilifanya mazungumzo na Rais wa Sudan, na alielezea masikitiko yake na nilimsisitizia umuhimu wa Serikali yake kufanya hivyo, kwa kuwa tukio hilo limetokea huko na hivyo waliofanya hivyo ni Wasudani,” alisema Rais Kikwete.
Alisema alimsisitiza, kwamba kwa kuwa mauaji hayo yamefanyika katika mamlaka ya Sudan, waliohusika wawe Waasia au Wasudani, lakini achukue hadhari zote kuwasaka.
Waziri Ulinzi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alisema Watanzania wamesikitishwa na mauaji hayo na inaweza kuwa mkakati wa kufifisha juhudi za UN kuleta amani.
“Wizara itatoa kila msaada kuwezesha maziko na kusaidia familia za marehemu na waliojeruhiwa,” alisema Nahodha.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Meja Jenerali Salum Mustapha Kijuu, Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu, alisema tukio hilo linasikitisha na ni msiba wa Taifa kwa kuwa askari hao walikufa kazini na ni mashujaa.
Katika eneo hilo, miili ya wanajeshi hao iliingia kila mmoja kwa gari maalumu la Jeshi na kupokewa na maofisa wa JWTZ na kupelekwa sehemu iliyoandaliwa kuagwa. UN itatoa medali kwa kila askari, kwa kutambua mchango wao.
No comments:
Post a Comment