WAHITIMU WA VYUO VIKUU NCHINI SASA KUKOPESHWA FEDHA ZA KUANZISHA MIRADI ILI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA UKOSEFU WA AJIRA...!!
WASOMI watakaohitimu vyuo vya elimu ya
juu nchini kuanzia mwaka huu watakopeshwa mabilioni ya fedha ili
waanzishe miradi itakayowawezesha kujiajiri. Hatua hiyo ni matokeo ya
Programu ya Wizara ya Kazi na Ajira inayolenga kukuza ajira kwa vijana
wahitimu wa vyuo hivyo, kwa kushirikiana na vya elimu ya juu, taasisi za
fedha na wabia wa maendeleo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji
wa Wizara hiyo, Ridhiwani Wema alisema, Sh bilioni 54 zitahitajika
kufanikisha miradi 1,000 itakayotekelezwa kwa awamu tatu kwa miaka
mitatu ya utekelezaji. Kwa mujibu wa Wema, kati ya fedha hizo, Sh
bilioni 4.4 ni za mafunzo na kuandaa vijana ili wakopesheke na Sh
bilioni 50 zitakuwa dhamana.
"Lengo la
kuanzisha programu hii ni kuongeza fursa za ajira 30,000 za moja kwa
moja kwa wasomi hao kwa kipindi hicho. Tunaamini miradi watakayoanzisha
itafanya wajiajiri na kuajiri wengine.
"Katika kuhakikisha programu hii
inafanikiwa, Serikali imekubaliana na Benki ya CRDB kutoa mikopo kwa
vijana, mara utekelezaji utakapoanza rasmi. Utaanza kwa kuendeleza
programu ya mfano iliyoanzishwa na Idara ya Kilimo, Uchumi na Biashara
katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)," Wema alisema.
Alisema, baada ya hapo, wahitimu wa vyuo
vingine vya elimu ya juu nao watafikiwa na kuandaliwa vizuri kwa
mafunzo ili wawe wajasiriamali kupitia miradi watakayoianzisha kwa
kutumia mikopo watakayopewa. Wema alifafanua kuwa wahusika watalazimika
kuandika mapendekezo ya miradi yao ambayo yataangaliwa na kupangiwa
kiasi cha fedha, ili waweze kukopeshwa tayari kwa kuanza kuitekeleza.
"Miradi itakayoanzishwa itatoa mnyororo
mzima wa thamani, kwa mfano mradi wa alizeti na ukamuaji mafuta.
Tumejiridhisha kuwa miradi hiyo itapunguza wimbi la vijana kukimbilia
mijini, kwa sababu itakuwa ikitekelezwa katika maeneo watakakokuwa
wahitimu hao ambayo si ya mjini pekee," alisema.
Wema alifafanua kuwa katika awamu ya
kwanza vijana 600 kutoka SUA watahusika kumiliki miradi 200 ya kujiajiri
na kuajiri wahitimu wengine 5,400, wakati katika awamu ya pili, vijana
900 kutoka vyuo vingine wataanzisha miradi 300. Kwa maelezo yake, awamu
ya tatu itahusisha wahitimu 1,500 wa vyuo vingine ikiwamo VETA
itakayokuwa na miradi 500 itakayozalisha ajira 13,500.
"Hivyo ndivyo tutakavyotumia programu
hii kupunguza tatizo la ajira na kuhakikisha wanaoandika mapendekezo
yenye ushawishi na yanayoelezea miradi inayotekelezeka watakopeshwa,"
alisema na kuongeza kuwa muda utakapofika, wahitimu wataandikishwa na
kutambuliwa kupitia mikoa na wilaya wanamoishi.
Watapeliwa ajira Wakati mikakati ya
ajira ikiwekwa ili kukomboa vijana wasomi nchini, Jeshi la Polisi Dodoma
linamshikilia Mariam Tawakali (28) akidaiwa kutapeli wahitimu wa vyuo
vikuu kwa ahadi ya kuwapa kazi ya kuandikisha wananchi wanaotarajiwa
kupewa vitambulisho vya uraia chini ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA).
Hayo yalithibitishwa jana na Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime akisema Mariam alikamatwa juzi
katika Barabara ya Sita, Dodoma, baada ya Polisi kupata taarifa kutoka
kwa raia wema.
Alisema mtuhumiwa alikutwa na
vitambulisho vitano vyenye majina tofauti ya Mariam Tawakali na Monica
Emmanuel Ngaso (28), mkazi wa Nkuhungu, Dodoma.
Miongoni mwa vitambulisho hivyo ni cha
Mkutano Mkuu wa CCM, wa Novemba 11-13, mwaka jana ambapo kazi yake
ilionesha kuwa ni mhudumu.
Kingine ni cha kampuni ya Thaker Singh
Coast Action chenye jina la Monica Emmanuel Ngaso, kazi Katibu Muhtasi,
nacho kitambulisho cha New Dodoma Hotel chenye jina la Mariam Tawakal
kazi yake Katibu Muhtasi na cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima chenye
jina la Mariam Tawakali, kikionesha ni mwalimu wa taasisi hiyo kijijini
Chamwino.
Kamanda Misime alisema Mariam
alitangazia wananchi, kwamba kazi ya kuandikisha vitambulisho vya uraia
kwa Dodoma itaanza mwezi ujao.
Pia waliwaeleza kuwa atakayehitaji kazi
hiyo awasilishe maombi kwake akiambatanisha vyeti vya elimu ya sekondari
au chuo, picha za vitambulisho na fedha taslimu Sh 110,000 za
kiingilio. Aidha, aliwaambia atakayepata nafasi atalipwa mshahara wa Sh
400,000 kwa mwezi kwa miezi mitatu ambapo kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Alisema mtuhumiwa huyo alifanikiwa
kukusanya vyeti, picha na fedha kwa wananchi 29 wengi wao wakiwa
wahitimu wa vyuo vikuu mwaka huu.
Kamanda Misime alisema Polisi inatoa
hadhari kwa wananchi kuwa makini na wanaofanya vitendo hivyo na kuwataka
kutoa taarifa mapema wanapotilia shaka watu wa aina hiyo ili hatua za
kuwadhibiti zichukuliwe mapema.
Alitaka wananchi kuelewa kuwapo matapeli
wanaobuni miradi ya kujipatia fedha kwa udanganyifu na kuwataka
kuchukua hadhari mapema kwa kukataa kurubuniwa ajira na kutoa fedha bila
kuthibitisha.
Alisema Polisi inafuatilia kuona uhalali
wa vyeti vya wanafunzi hao wa vyuo vikuu na kuona ni kosa gani Mariam
atashitakiwa nalo. Pia alitaka waliotapeliwa kufika Polisi kutoa
ushahidi kabla ya kesi haijafikishwa mahakamani.
Imeandikwa na Namsembaeli Mduma, Dar na Sifa Lubasi, Dodoma.
No comments:
Post a Comment